YANGA KUTUPA KARATA YAKE TENA LEO - VYANKENDE.COM

Breaking

Post Top Ad

Millionaire  Ads

Thursday, 8 June 2017

YANGA KUTUPA KARATA YAKE TENA LEO

MABINGWA wa Ligi Kuu ya soka Tanzania bara, Yanga wanashuka dimbani leo kuivaa AFC Leopards ya Kenya katika nusu fainali ya Kombe la SportPesa kwenye uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam.
Yanga ilifikia hatua hiyo baada ya kuwatoa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Kenya, Tusker katika mchezo wa kwanza wa mtoano kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya kucheza dakika 90 na kutoka suluhu.
Timu hiyo inatarajiwa kubeba bendera ya Tanzania baada ya kubaki peke yake kwenye michuano hiyo nyingine zikitolewa. Timu nyingine, Jang’ombe Boys ya Zanzibar ilitolewa baada ya kupata kipigo cha mabao 2-0 kwa Gor Mahia ya Kenya.
Pia mabingwa wa Kombe la FA, Simba walitolewa na timu ya daraja la kwanza, Nakuru All Stars ya Kenya kwa penalti 5-4 baada ya kutoka suluhu dakika 90. AFC Leopards ilifikia nusu fainali baada ya kuwatoa Singida United kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika kipindi cha dakika 90.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi ameutabiri mchezo huo kuwa utakuwa ni mgumu kutokana na kila mmoja kuwa na uchu wa kufika fainali za michuano hiyo. Alisema kwa jitihada ambazo kikosi chake chenye vijana wengi walizionesha katika mchezo wa kwanza, anaamini mambo yatakuwa mazuri pia katika mchezo huo.
Kocha wa AFC Leopards anayeifahamu Yanga vizuri, Mtanzania Denisi Kitambi alisema mchezo wa leo muhimu kwao kushinda hivyo na wamejipanga vizuri. Alisema pamoja na Yanga kuwa na mashabiki wengi, hawatishiki zaidi ya kufanya maandalizi mazuri ili washinde.
Mchezo mwingine wa nusu fainali utakaochezwa ni wa Gor Mahia dhidi ya Nakuru All Stars zote za Kenya. Kocha wa Nakuru All Stars, Maina George alisema anataka kuweka historia mpya kwa kuzitoa timu zote kubwa kwenye michuano hiyo na kucheza fainali kutokana na kuwa anataka kucheza na Everton ili kutumia fursa hiyo kuwaonesha vijana wake.
Kocha wa Gor Mahia, Zedekiah Otieno alisema wanajipanga dhidi ya Nakuru na imani yao ni kushinda na kufika fainali. Fainali ya michuano hiyo inatarajiwa kuchezwa Jumapili ya wiki hii ambapo bingwa atakutana na Everton inayoshiriki Ligi Kuu ya England Julai 13, mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Michuano hiyo inadhaminiwa na Kampuni ya michezo ya kubahatisha, SportPesa inayoidhamini Everton katika Ligi Kuu ya Uingereza na ina biashara zake Kenya pia.

No comments:

Post Bottom Ad

Pages