USAJILI 2017/18 …UTAONDOA DONDA SUGU LA SIMBA, AZAM NA YANGA? - VYANKENDE.COM

Breaking

Post Top Ad

Millionaire  Ads

Tuesday, 13 June 2017

USAJILI 2017/18 …UTAONDOA DONDA SUGU LA SIMBA, AZAM NA YANGA?


SOKO la wachezaji kipindi hiki cha usajili linazidi kushika hatamu huku timu ya Azam ambayo ni miongoni mwa timu zenye uwezo wa kifedha, ikionekana kufanya kweli hadi sasa katika eneo hilo.

Azam tayari imewasajili wachezaji watatu wakali waliofanya vizuri msimu uliopita, ambao ni mastraika Mbaraka Yusuph, Wazir Junior na kiungo Salmin Hozza.

Kutua kwa mastraika hao wawili ndani ya kikosi cha Azam inaonyesha namna gani Wanalambalamba hao walivyodhamiria kuifanya timu iwe tishio kwenye safu yao ya ushambuliaji kutokana na ubutu wa idara hiyo kwa misimu kadhaa.

Huku kwa upande wa Simba wakiwa tayari wamewavuta wachezaji wawili pekee beki wa kushoto, Jamal Mwambeleko na beki wa kati Yussuf Mpili.

Lakini kwa mabingwa Yanga bado tetesi zinaendelea kuchukua nafasi kwani hadi sasa hakuna mchezaji ambaye wameweka wazi kumalizana naye.

Katika timu hizo tatu kupitia wadau wa soka wakiwamo baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi, kama vile mameneja na makocha wasaidizi, walikiri kuwa kwa misimu kadhaa vikosi vyao vilipwaya katika nafasi moja au zaidi.

Kutokana na kipindi hiki ambacho ndicho cha kufanya maboresho ya vikosi ni muda sahihi wa kufanya usajili wa tija ambao utaendana na matakwa ya sehemu husika ambao huenda ikawa mwarobaini.

Ujio wa Mbaraka na Wazir ndani ya kikosi cha Azam ni kwa ajili ya kuongeza uhai katika safu ya ushambuliaji, kwani katika misimu kadhaa kumekuwa butu ikiwamo msimu uliopita.

Msimu huo nahodha wao wa zamani, John Bocco, alifunga mabao nane, akifuatiwa na Shaban Idd akitikisa nyavu mara saba, wakiachwa kwa mbali na mastraika wa Yanga, Obrey Chirwa na Simon Msuva.

Tukigeukia kwa Simba, iko wazi pia tatizo lao sugu kwenye kikosi ni safu ya ushambuliaji, licha ya kuwa na viungo wenye uwezo wa juu walioonekana kutengeza nafasi nyingi za wazi.

Mastraika waliofanya vizuri Simba kwa kuwa na wastani mzuri wa kuingia kimiani ni Amisi Tambwe (2012/13) na Hamis Kiiza (2015/16) kila moja akifunga mabao 19.

Ni tofauti na msimu uliopita ambapo mshambuliaji tegemeo, Laudit Mavugo alifunga mabao sita pekee akizidiwa na kiungo Mzamiru Yassin aliyepachika mabao nane.

Yanga pamoja na kufanikiwa kutetea ubingwa wao kwa mara ya tatu mfululizo, wamekuwa na mapungufu ya kiungo mkabaji kwa misimu kadhaa licha ya uwepo wa Thabani Kamusoko na Juma Said Makapu.

Kwa kulibaini hilo, walikuwa kwenye mipango ya kumsajili mzawa, Kenny Ally, lakini kwa bahati mbaya zaidi Singida United ikamvuta fasta hatua inayowafanya Yanga waendelee kusaka kiungo mwenye uwezo wa juu kucheza kama namba sita asili.

Nyota mwingine aliyekuwa akifukuziwa na Yanga, ni Salmin Hoza aliyenaswa na Azam FC, ambao inaelezwa Yanga rada zao zitaangalia zaidi ya mipaka ya Tanzania.

Suala muhimu la kusubiri ni kama timu hizi tatu zenye uchumi mzuri zitatimia dirisha hili la usajili 2017/18 kupata wachezaji mahiri na watakaoendana na falsafa zao.

No comments:

Post Bottom Ad

Pages