Tunahitaji akili kuwaelewa Azam, sio ‘mapovu’ - VYANKENDE.COM

Breaking

Post Top Ad

Millionaire  Ads

Thursday, 8 June 2017

Tunahitaji akili kuwaelewa Azam, sio ‘mapovu’

VIONGOZI wa klabu ya Azam kwa akili zao timamu bila kushawishiwa na yeyote yule wameamua kuja na sera ya kupunguza matumizi yasiyokuwa na ulazima klabuni mwao. Hawajaishia kupunguza matumizi tu, wameamua kupunguzana na wao wenyewe.
Inahitaji zaidi ya akili kuwaelewa Azam kwa hiki wanachokifanya sasa. Kuna watu si wachezaji, wala viongozi, lakini waliendesha maisha yao kupitia Azam. Watu wa namna hii ni miongoni mwa watakaokuwa waathirika wa upepo huu wa mabadiliko ndani ya Azam.
Hii ni moja ya taarifa mbaya zaidi kuisikia ikipenya kwenye ngoma za masikio yao wale waliopunguzwa. Upepo huu wa mabadiliko hautawakuta wale walioishi kwa ajili ya upambe ndani ya timu, umewakumba hadi wachezaji. Upepo huu hauwezi kuacha watu salama. Wahusika lazima wajisikie vibaya kwa namna yoyote ile.
Muda huu tunaotafakari juu ya mambo yanayoendelea ndani ya Azam na kuwaonea huruma waliopewa mkono wa kwaheri, tujiulize tuliwahi kuzionea huruma fedha za wamiliki?
Fedha nyingi zimeliwa Azam kwa matumizi yasiyokuwa na kichwa wala miguu. Timu ilisajili wachezaji wengi wenye ubora wa kawaida na wajanja wachache 'kupiga vya juu'. Rais wa Tanzania awamu ya Tano, John Pombe Magufuli, anapenda kuwaita jina la 'wapiga dili' watu wa namna hii.
Kuna watu wanatajwa kugawana hadi mishahara na wachezaji. Hivi bado hatuzionei huruma zile fedha za Mzee Bakhresa ambaye alikuja na nia nzuri ya kukuza na kuendekleza soka la Tanzania, lakini wajanja wakaharibu?
Siku zote upepo wa mabadiliko haujawahi kuacha watu salama. Hali iliyoko sasa ilikuwa lazima itokee. Azam wanatakiwa kuwa timu ya kuigwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Nafahamu kuna watu wana masilahi na Azam kwenye kila kitu kinachofanyika ndani ya timu, lakini ule muda wa kusafiri na timu, kuvuna posho ‘mlima’ na kupenyeza maneno kwa bosi umefikia kikomo. Karibuni tutaiona Azam ya tofauti.
Shida ya matatizo yote inaanzia kwa timu kutojiendesha kibiashara. Matumizi ya timu yamekuwa makubwa tofauti na kitu anachovuna mwekezaji. Unadhani mwekezaji angekaa kimya siku zote kushuhudia mabilioni ya shilingi yakizidi kuteketea matumboni mwa wajanja? Ilikuwa ngumu kuliona hili likiendelea.
Inasikitisha kwa kila mmoja aliyepitiwa na upepo huu wa mabadiliko, hasa kwenye hali ngumu ya maisha kama iliyoko sasa, lakini hakuna njia nyingine ya kupunguza matumizi klabuni hapo zaidi ya kufanya hivyo.
Ujasiri wa kujivisha mabomu na kufanya walichokifanya wamiliki wa Azam na mmoja wa kiongozi wake, si jambo dogo hata kidogo. Hili ni jambo linaloweza kupoteza maisha ya mtu katika hali ya mzaha. Jambo hili limegusa masilahi ya watu na familia zao.
Ni jambo la kawaida hivi sasa kwenye mikusanyiko ya watu wa mpira mjini kusikia zigo la lawama juu ya hili akitwishwa Abdul Mohamed, yule Meneja Mkuu wa klabu.
Kila aliyeguswa na wimbi la mabadiliko akiwa kijiweni anamuona Mohamed kama ndiyo chanzo cha mabadiliko ya yote haya, lakini ukweli wa mambo ni wamiliki wenyewe kuchoka jinsi klabu inavyoendeshwa. Inachosemekana alichokifanya Mohamed ni kutengeneza muundo wa timu inavyotakiwa kuwa kuanzia msimu ujao.
Kitendo hiki kinafanya tumuone Mohamed kiumbe tofauti mbele ya mboni zetu za macho. Tunatakiwa kufahamu Mohamed hana nguvu ya kuagiza mchezaji fulani abaki, kiongozi fulani abaki na komandoo fulani abaki. Hana hiyo nguvu. Ikizingatiwa walioondoka na watakaoondoka wote aliwakuta klabuni. Huyu Mohamed ana nguvu gani kiasi hiki mbele ya wamiliki?
Kama mtaalamu wa masuala ya uendeshaji klabu, Mohamed alitoa ushauri wake kama meneja jinsi klabu inavyotakiwa kuendeshwa na wamiliki wakaona sahihi. Hii haifanyi tumuone kama ameharibu maisha ya watu maana yeye si mtu wa mwisho anayeweza kushika kalamu nyekundu na kusaini mkataba wa mtu anayetakiwa kuondoka au kuingia, hii mikono mirefu kwa Mohamed inatoka wapi?
Ili mpira usonga tunahitaji kuwaunga mkono Azam kwenye hili wanalofanya sasa, japo si suala jepesi. Azam inapaswa kuwa klabu ya kuigwa na timu nyingine, lakini sio kuwa klabu ya watu kwenda kuchota fedha za ubwete.
Azam kugotea hapa iliko ni kutokana na kujaza watu wengi wenye sura ya ubinafsi. Hali ya ubinafsi iliyotawala ndiyo imeifikisha hapa tofauti na awali ambao tulijua uwepo wao utabadilisha muundo mzima wa soka la Tanzania.
Azam ina kila kitu kwenye maisha yake, kwanini iko katika sura hii ya simanzi? Walichokifanya wamiliki tulitakiwa kukiona misimu mitano iliyopita, lakini haijachelewa sana. Mpira ni biashara inayolipa vizuri na kuajiri watu wengi kwa wakati mmoja, lakini Azam haikuwa imeufanya mpira sehemu ya biashara, iliufanya mpira kama sehemu ya burudani kwa wamiliki kukutana na kunywa kahawa nyakati za usiku kwenye uwanja wa Chamazi.
Muda huu ambao wamiliki wake wameamua kufanya kweli kwa kutoa nafasi kwa vijana waliokulia ndani ya timu yao B, tunahitaji kuwaunga mkono na sio kuwapuuza. Wamiliki wamepoteza fedha nyingi kuifanya Azam ifike hapa, japo haikutakiwa kuwa hapa. Ilitakuwa kuwa mbali zaidi na zaidi.
Kuwatenganisha mabosi wa Azam na rafiki zao walioko ndani na nje ya timu inahitaji kujivisha ngozi ya simba. Haya maneno tunayoyasikia sasa kutoka upande wa pili yamegusa masilahi yao binafsi ndiyo maana tunayasikia.
Hakuna aliyeko salama watu wa ndani ya Azam na pembezoni mwa Azam. Wote wamekalia nusu nusu, hakuna aliyejitawala kukaa vizuri na kutulia.
Katikati ya wiki iliyopita kaka yangu Japhar Iddy Maganga ambaye ni ofisa habari wa Azam, aliitisha mkutano wake na waandishi wa habari, Mzizima jijini Dar es Salaam na kuzungumza mengi ya Azam na mwisho akasema, hata yeye hayuko salama. Kauli ya Japhar si ya kuipuuzia. Ni kauli ya kujifikirisha mara mbili mbili.
Binafsi nimewaelewa wamiliki wa Azam kwa hiki wanachokifanya ndani ya timu yao. Inahitaji kujivalisha ‘uchizi’ na kutumbua majipu haya yaliyotuama muda mrefu pale kwenye viunga vya Chamazi.
Si vibaya na sisi wadau wa nje ya Azam, tuanze kuwaelewa wamiliki kwa kila wanalofanya na tuwaunge mkono kwa ajili ya maendeleo yao na maendeleo ya soka la Tanzania.

No comments:

Post Bottom Ad

Pages