REKODI KUIBEBA TUSKER DHIDI YA YANGA. - VYANKENDE.COM

Breaking

Post Top Ad

Millionaire  Ads

Monday, 5 June 2017

REKODI KUIBEBA TUSKER DHIDI YA YANGA.Pazia la ligi ya SportPesa kufunguliwa leo nchini katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kwa michezo miwili. Mchezo wa kwanza utaanza saa nane kamili mchana kati ya Singida United na AFC Leopard na saa 10:00 jioni mabingwa wa ligi kuu nchini Kenya Tusker FC watavaana na mabingwa wa Tanzania Yanga SC.
Michezo yote miwili ina mvuto wa aina yake leo. Wengi watataka kuwaona Singida United ambao wamepanda ligi kuu hivi karibu na kufanya usajili wa kufuru wataikabili vipi AFC Leopards moja ya timu kongwe Afrika Mashariki lakini ni ukweli usiopingika mechi ya jioni kati ya Yanga na Tusker ndio gumzo kuu katika ufunguzi wa michuano hii mipya ya SportPesa Super league ambayo bingwa atanyakua kitita cha dola 30,000 za kimarekani karibu shilingi milioni 66 za kitanzania na mshindi wa pili dola 20,000/-.
Yanga wana kazi ya ziada leo mbele ya mabingwa hao wa Kenya ambao rekodi yao ya hivi karibuni katika ligi kuu nchini Kenya ( KPL ) inayodhaminiwa na waandaaji wa michuano hii , SportPesa inaonesha ni jinsi gani Tusker walivyo moto wa kuotea mbali.
Katika mechi zao tano za mwisho katika ligi kuu kabla ya kuja hapa nchini, wameshinda mechi zote. Tarehe 6 Mei , waliwafunga Kakamega 1-0 , tarehe 10 Mei ugenini dhidi ya Zao FC waliwatungua 2-0 . 14 Mei wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani waliwabugiza 2-1 Sony Sugar na tarehe 20 Mei wakiwa ugenini dhidi ya timu ngumu ya Mathare United waliwachapa 2-0.
Mchezo wa mwisho wa Tusker FC katika ligi kuu nchini Kenya kabla ya ligi kusimama kwa mechi za timu ya taifa ( Harambee Stars ) , waliwapiga 1-0 AFC Leopards ambao wataikabili Singida United mechi ya kwanza leo majira ya saa 8:00 mchana .
Rekodi hii ya Tusker FC inadhihirisha jinsi gani walivyo na beki imara na safu ya ushambuliaji makini. Tofauti na Yanga SC ambao wapo katika mapumziko ya kuanza msimu mpya wa ligi kuu , Tusker FC bado wapo katika ligi na ni dhahiri bado rhythm yao kimbinu ipo juu na watawapa upinzani mkali Yanga S.
Kama ilivyo kwa Yanga SC leo kuwakosa nyota wake kadhaa baada ya wengi wao kuitwa katika timu zao za taifa , pia baadhi ya wachezaji wa Tusker FC wapo katika timu ya taifa ya Kenya.
Mchezo wa mwisho wa Yanga SC ni mechi ya kirafiki jijini Arusha dhidi ya timu ya ligi daraja la pili AFC mchezo ambao Yanga walishinda 3-0. Baada ya mchezo huo uliopigwa juma lililopita , Yanga walikuwa mapumzikoni na wameanza rasmi mazoezi ijumaa kwa ajili ya mechi ya leo . Maandalizi haya yanakupa picha kamili jinsi gani Yanga SC watakavyokuwa na kazi ya ziada kuikabili timu ambayo bado ipo katika ligi .
Kocha msaidizi wa Yanga SC, Juma Mwambusi amesema katika kufidia upungufu wa wachezaji wake ambao wapo katika timu zao mbalimbali za taifa , amewapandisha wachezaji watano wa timu B ambao kwa takribani wiki 2 wamekuwa wakifanya mazoezi na timu kubwa na wengi wao ndio walicheza mechi ya kirafiki dhidi ya AFC jijini Arusha.
” tutawatumia vijana wetu wa timu B na wachezaji wote waliobaki timu kubwa katika michuano hii SportPesa. Ni vijana wazuri na wameonesha kazi nzuri toka tumewachukua timu B” alisema kocha huyo akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi tu baada ya mazoezi.
Baadhi ya wachezaji hao ni kiungo mkabaji Maka Edward, mlinzi wa kushoto Mohamedi Ali na washambuliaji Samweli Greyson na Festo Greyson .
Wachezaji wa timu kubwa ambao wanatarajiwa kuwaongoza vijana hawa leo dhidi ya Tusker ni walinda milango ; Deogratius Munishi na Ali Mustafa.
Walinzi; Andrew Vicent , Juma Abdul, Haji Mwinyi, Nadir Haroub , Kelvin Yondani, Vincent Bossou na Pato Ngonyani.
Safu ya kiungo ni kinda Yusufu Mhilu , Juma Makapu , Geofrey Mwashuiya, Juma Mahadhi na Babu Seif.
Washambuliaji ni Emanuel Martin na Mateo Antony na Mrisho Ngassa.
By Samuel Samuel

No comments:

Post Bottom Ad

Pages