MFAHAMU KOCHA MPYA WA BARCELONA ERNESTO VALVERDE - VYANKENDE.COM

Breaking

Post Top Ad

Millionaire  Ads

Friday, 2 June 2017

MFAHAMU KOCHA MPYA WA BARCELONA ERNESTO VALVERDECATALONIA, Hispania

MIAMBA ya soka Hispania, Barcelona, imemtangaza Ernesto Valverde, kuwa kocha wao mpya akienda kurithi mikoba ya Luis Enrique ambaye ameaga rasmi Catalunya baada ya kuinoa kwa miaka mitatu ya mafanikio.

Enrique alifanikiwa kunyakua mataji tisa akiwa na Barca, mafanikio makubwa yakiwa ni katika La Liga.

Lakini kutokana na yeye mwenyewe kuona huu sasa ni wakati wa kuiaga timu baada ya kuipa mataji, Enrique alitangaza miezi michache iliyopita kuwa huu msimu uliomalizika wiki chache zilizopita ni wa mwisho kwake.

Na baada ya kuondokewa na mkali huyo, Barca ilimtangaza Valverde kuwa kocha wao mpya wa msimu ujao.

Februari 9, 1964, Valverde alikuja duniani. Ndani ya mji wa Viandar de la Vera, Hispania, ndiko alikokulia.

Alianza kusakata soka lake kama mshambuliaji katika timu za Deportivo Alaves na Sestao Sport Club kabla ya kupelekwa RCD Espanyol mwaka 1986.

Akiwa Espanyol, Valverde alicheza mechi 43 za ligi na kufunga mabao saba na alionja uchungu (kama si utamu) wa michuano ya UIaya, ambapo kikosi chake kilibamizwa na Bayer Leverkusen kwenye fainali ya Uefa Cup kwa mikwaju ya penalti.

Zaidi ya kuitumikia Espanyol, Valverde alizichezea timu za Barcelona (akitwaa mataji ya Copa del Rey na Kombe la Washindi la Uefa), Athletic Bilbao, Olympiacos, Valencia na Villareal. Jumla ya mechi 320 na kufunga mabao 77.

Ni mmoja kati ya makocha wenye uzoefu mkubwa na soka la Hispania, akiwa na uzoefu wa miaka 10 wa kufundisha soka nchini humo.

Aidha, Valverde ni kocha mwenye historia ya kuifundisha Bilbao kwa muda mrefu, ambapo amekuwa kocha wa timu hiyo kwa zaidi ya mechi 300 katika vipindi viwili tofauti vya miaka miwili na minne.

Akiwa na Bilbao, Valverde aliiongoza timu hiyo kunyakua taji la Spanish Super Cup na kuondoa ukame wa miaka 31 bila kombe baada ya kuichapa Barçelona jumla ya mabao 5-1 mwaka 2015.

Kocha huyo pia alifanikiwa kuipeleka Bilbao kwenye michuano ya Ulaya kwa miaka minne mfululizo.

Kama hiyo haitoshi, Valverde alifanikiwa kuifundisha Espanyol kwa mafanikio; akiiongoza timu hiyo kutinga fainali ya michuano ya Ulaya 2007 (UEFA Cup) waliyofungwa na Sevilla kwa mikwaju ya penalti.

Zaidi ya kufundisha soka Hispania, Valverde pia ana rekodi zake nje ya taifa hilo, akifanikiwa kubeba mataji matatu ya ligi na klabu ya Ugiriki, Olympiacos.

Ujio wa Valverde ni mwendelezo wa Barcelona kuwapa vibarua makocha ambao waliwahi kuwemo ndani ya klabu hiyo zamani na wanaofahamu tamaduni zake.

Ilianza na Johan Cruyff, Pep Guardiola na Enrique, sasa imerudi kwa Valvderde ambaye aliitumikia timu hiyo akiwa mchezaji msimu wa 1988–90.

Valverde pia ni mjuzi wa kuinua vipaji vya wachezaji, sambamba na kutoa nafasi kwa vijana kuonesha walichonacho kwenye kikosi cha wakubwa, ambapo akiwa na Bilbao vijana waliong’ara zaidi chini yake msimu huu ni Kepa Arrizabalaga, Iñaki Williams na Yeray Álvarez.

Kutokana na hilo, Barca imepata mtu sahihi ambaye ataangaza jicho lake vyema kwenye akademi maarufu ya La Masia ambayo kwa miaka michache ya hivi karibuni imetetereka.

Ni kocha anayependa kufundisha soka la kukaba na kushambulia kwa kasi. Ni mbinu iliyomfanya aiongoze Bilbao kumaliza nafasi ya tano katika msimu wake wa kwanza tu akiwa kama kocha (2003/04) na aliporudi tena Bilbao 2013/14 akawaongoza kumaliza nafasi ya nne iliyowapa tiketi ya kucheza ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya miaka 16.

Ni kikosi ambacho kilicheza soka la kuvutia mno, mashambulizi ya kasi na umiliki mzuri wa mpira kwa kila mchezaji aliye kwenye nafasi yake.

Ndicho kikosi kilichokuja kufundishwa na Marcelo Bielsa na kuonekana imara, kwani kocha huyo aliongeza ufundi wa safu ya ulinzi lakini kazi kubwa ilishafanywa na Valverde.

Barcelona inajulikana kwa matumizi makubwa ya mfumo wa 4-3-3, lakini hilo halitamzuia Valverde kubadili mifumo pale inapobidi.

Alipokuwa Espanyol, alibadili mno mifumo kutoka 4-4-2 hadi 4-2-3-1, akiwa Valencia alitumia 4-3-3 tu.

Aliporudi Bilbao, Valverde alitumia mifumo ya 4-2-3-1, 4-4-2 na 4-3-3 kutegemea na hali ya mchezo.

Pia, Valverde hana rekodi ya kusumbuliwa na udhaifu wa kutokuwa na umoja ndani ya kikosi, ingawa hakuwahi kuinoa timu yenye mastaa wenye hadhi tofauti kama Barca.

Robert Pires, Joan Capdevila, Marcos Senna, Julen Guerrero, Fernando Gago, Ever Banega, David Albelda, Ander Herrera na Aritz Aduriz wanasimama kama wachezaji waliowahi kuwa chini ya Valverde na kila alichowaelekeza walimsikiliza.

Anakumbukwa pia kwa ujasiri wake wa kushughulika na ukorofi wa Gago akiwa na klabu ya Valencia, lakini mashabiki wanajiuliza ataziba vipi pengo la Andres Iniesta ambaye amepungua kiwango?

Hilo sio shida kwake, kwani aliweza kuziba vizuri mapengo yaliyoachwa na nyota kama Andoni Iraola, Guerrero, Gorka Iraizoz, Carlos Gurpegi na Larrazabal katika timu za Valencia na Bilbao.

Source: Bingwa.co.tz

No comments:

Post Bottom Ad

Pages