SIMBA YAIPIKU YANGA KWA HILI... - VYANKENDE.COM

Breaking

Post Top Ad

Millionaire  Ads

Monday, 29 May 2017

SIMBA YAIPIKU YANGA KWA HILI...

Usikose kila siku kupata habari za michezo ndani na nje ya nchi kupitia simu yako kwa kudownload app yetu Bofya HAPA kudownload...


 Yanga haina ujanja wa kuwakwepa mahasimu wao wa jadi Simba.

Mabingwa hao wapya wa Tanzania Bara, Yanga, awali walielezwa kukwepa kukutana na Simba katika fainali ya Kombe la Shirikisho walipokubali kufungwa na Mbao FC bao 1-0.

Kipigo kutoka kwa Mbao FC kiliifanya Yanga kuutema Ubingwa wa Kombe la FA ambao waliutwaa msimu uliopita kwa kuilaza Azam FC mabao 3-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Baada ya kusemekana kuikwepa Simba, sasa Yanga haitakuwa na uwezo wowote kukwepa kukipiga na mahasimu wao Simba, kwani sasa timu hizo zitakutana kwenye mchezo wa awali wa fungua Dimba wa Ligi hiyo.

Kwa namna yoyote lazima miamba hiyo itakutana, kwani Simba wameshinda Kombe la Shirikisho ambalo mshindi wake anawakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, lakini pia imeshika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu, hivyo mchezo wa Ngao ya Hisani ambao huwa ni ufunguzi wa pazia la ligi kuu utazikutanisha timu hizo kwa vigezo vyote.

Kigezo cha kwamba mchezo huo unakutanisha mshindi wa kwanza na wa pili wa ligi, unazikutanisha Simba na Yanga na kigezo cha bingwa wa ligi na Mshindi wa FA vyote vinazikutanisha timu hizo mahasimu za Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana katika mchezo wa Ngao ya Hisani, ilikuwa mwaka 2011 na Simba kufanikiwa kutwaa ubingwa huo kwa kuwachapa wapinzani wao hao mabao 2-0, mabao ya Wekundu wa Msimbazi yakipachikwa wavuni na Haruna Moshi  ‘Boban’ na Felix Sunzu kwa mkwaju wa penalti.

Rekodi zinaonyesha kuwa Yanga ndio timu pekee ambayo imeshatwaa Ngao ya Hisani mara tano baada ya kucheza mechi nane za Ngao ya Jamii na kuwa timu pekee iliyochukua mara nyingi zaidi ikifuatiwa na Simba ambayo imechukua mara mbili.

Azam kwa sasa ndio wanashikilia taji la Ngao ya Hisani, lakini wameshalitema baada ya kushinda kuchukua Kombe la FA na Ligi Kuu kumaliza katika nafasi ya nne.

Mchezo huo ambao utafanyika Agosti, umeshagusa hisia za wachezaji kadhaa nyota wa timu hizo, ambapo kwa upande wa Yanga, nahodha msaidizi, Haruna Niyonzima amesema kama mambo yatakuwa vizuri basi angependa kuanza msimu vyema kwa kunyakua taji.

“Ni vyema kuanza msimu kwa mafanikio, vyovyote itakavyokuwa lakini nitafurahi kuona tunaanza msimu kwa kunyakua taji na si kupoteza mchezo,” alisema Niyonzima.

Kwa upande wake, Mshambuliaji mahiri wa timu hiyo, Donald Ngoma, alisema pamoja na masuala mengine ya usajili kutompa uhakika wa kubaki kikosini, lakini kwa vyovyote kama akiwepo hatapenda timu yake ipoteze mchezo huo muhimu wa ufunguzi wa ligi.

Wakati wakali hao wa Yanga wakisema hivyo, Winga kiboko ya Simba ambaye amekuwa akiogopwa na kutajwa na Wanayanga kila kona, Shiza Kichuya, amesema kama kawaida yake hufunga mabao muhimu na mechi muhimu kwa timu yake.

“Nimewafunga mara mbili na katika mchezo huo nitawafunga tena,” alisema Kichuya.

Winga huyo aliifunga Yanga bao la kusawazisha katika dakika ya 87 ya mchezo wa raundi ya kwanza Ligi Kuu uliomalizika kwa bao 1-1, pia akafunga bao la ushindi katika mchezo wa marudiano kwa mabao 2-1.

Mara ya kwanza Yanga kutwaa ubingwa huo ilikuwa ni mwaka 2001 ilipoanzishwa Ngao ya Hisani baada ya kuwafunga Simba mabao  2-1  magoli ya Wanajangwani hao yalifungwa na Edibily Lunyamila na Ally Yusuph ‘Tigana’, huku la  Simba likifungwa na  Steven Mapunda ‘Garincha’.

No comments:

Post Bottom Ad

Pages